Kile Unapaswa Kujua Kuhusu Mapenzi ya Jinsia Moja

Bonyeza hapa kupata mahojiano na mwanamme shoga na mwanamke msagaji kutoka Tanzania. Bofya hapa kujifunza zaidi kuhusu jinsia.

Mwelekeo wa kimapenzi ni nini?

Mwelekeo wa kimapenzi humaanisha muundo wa kudumu wa kimhemko, kimahaba, na/au mivuto ya kimapenzi kwa wanaume, wanawake, au jinsia zote. Mwelekeo wa kimapenzi unaweza kuwa wa toka kuvutiwa na jinsia tofauti tu hadi kuvutiwa na jinsia moja tu. Japokuwa, mwelekeo wa kimapenzi kwa kawaida hujadiliwa katika makundi matatu: mpenda jinsia tofauti (kuwa na mvuto kwa wahusika wa jinsia nyingine), shoga/msagaji (mwanaume anayevutiwa na wanaume/mwanamke anayevutiwa na wanawake), na mpenda jinsia mbili (mwanaume au mwanamke anayevutiwa na jinsia zote mbili; “bisexual”).

Watu hujua vipi kama wao ni wasagaji, mashoga, au wapenda jinsia mbili?

Utajua wakati utapojua. Inaweza kuchukua muda, na hakuna haja ya kuharakisha. Vivutio vya msingi ambavyo huunda msingi wa mwelekeo wa kimapenzi wa watu wazima kwa kawaida huibuka katikati ya kati ya utoto na mwanzo za kubalehe. Watu tofauti walio wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili wana uzoefu tofauti sana juu ya mwelekeo wao wa kimapenzi. Watu wengine wanajua kuwa wao ni wasagaji, mashoga, au wapenda jinsia mbili kwa muda mrefu kabla hawajaanza uhusiano na watu wengine. Watu wengine hujihusisha na vitendo vya kimapenzi kabla ya kuchukua msimamo juu ya mwelekeo wao wa kimapenzi. Ubaguzi na unyanyapaa hufanya iwe vigumu kwa watu wengi kufuata mwelekeo wao wa kimapenzi unao watambulisha, hivyo, kujitangaza kuwa shoga, msagaji, au mpenda jinsia mbili kunaweza kuwa mchakato wa taratibu.

Nini husababisha mtu kuwa na mwelekeo fulani wa kimapenzi?

Hakuna makubaliano kati ya wanasayansi juu ya sababu halisi ambazo humfanya mtu kuwa na mwelekeo wa kupenda jinsia tofauti, shoga, kupenda jinsia mbili, au msagaji. Wengi wanafikiria asili pamoja na mazingira vinachangia. Ila, tunachojua ni kwamba watu hawachagui mwelekeo wao ya kimapenzi kama tusivyochagua rangi zetu za ngozi.

Ubaguzi na unyanyapaa huchangia nini kwenye maisha ya watu walio wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili?

Ni wazi kuwa, watu walio wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili hukumbana na ubaguzi, unyanyapaa, na ukatili mkubwa kwa sababu ya mwelekeo wao wa kimapenzi. Wengi hukumbana na ubaguzi kwenye mashule, vyuo vikuu, na sehemu zao za kazi, wananyimwa upataji huduma za afya na haki, na hupata msaada mdogo kutoka kwa wanafamilia na marafiki. Wakati hili ni tatizo la kiulimwengu, hali ni mbaya sana hasa katika sehemu kubwa za Afrika. Utafiti wa kidunia uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew mnamo mwaka 2007 uligundua kuwa ni 3% tu ya Watanzania, Wakenya, na Waganda wanaamini kuwa ushoga unapaswa kukubalika. Matendo ya mwelekeo (mvuto) wa jinsia moja huchukuliwa kuwa ni uhalifu katika nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), isipokuwa Rwanda, na adhabu yake ni kifungo cha muda mrefu gerezani. Matokeo yake, ni wachache tu walio wazi kuhusu mwelekeo wao wa kimapenzi, wakati wengi wanalazimishwa kuishi maisha ya usiri na uwongo, ili waendane na dhana potofu za kimaadili.

Ni nini athari za kisaikolojia za ubaguzi na unyanyapaa?

Chuki dhidi ya mashoga (“homophobia”) ni kubwa na ina madhara makubwa kwa afya ya akili na ustawi wa watu walio wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili, haswa ikiwa wanajaribu kuficha au kukataa mwelekeo wao wa kimapenzi. Ubaguzi, unyanyapaa, na ukatili ni vyanzo vikuu vya mafadhaiko kwa wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili. Wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili wako katika hatari kubwa ya kujiua kuliko wenzao wanaovutiwa na jinsia tofauti.

Watu wanaweza kufanya nini kupunguza ubaguzi na unyanyapaa dhidi ya wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili?

Wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili wanaotaka kusaidia kupunguza ubaguzi na unyanyapaa wanaweza kuwa wazi kuhusu mwelekeo wao wa kimapenzi, huku wakichukua tahadhari muhimu ili kuwa salama kadiri iwezekanavyo. Wapenzi wa jinsia tofauti wanaotamani kusaidia wanaweza kufika sehemu ya kujua wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili, na wao wanaweza kufanya kazi na mashirika husika kupambana na unyanyapaa.

Je mapenzi ya jinsia moja ni tatizo la kiakili, ugonjwa, ulemavu, jambo lisilo la asili, au lisilo la kawaida?

Hapana. Mielekeo ya usagaji, ushoga, na kupenda jinsia mbili, sio ugonjwa. Miongo mingi ya utafiti na uzoefu ya kitabibu imepelekea mashirika yote ya afya na ya afya ya akili kuthibitisha kuwa mielekeo hii huwakilisha ni hali za kawaida za maisha ya mwanadamu. Mahusiano ya jinsia moja, kama yalivyo mahusiano kati ya mwanaume na mwanamke, ni hali za kiasili na kiafya za muunganiko wa binadamu. Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) liliondoa ushoga kutoka kwenye orodha yake ya magonjwa ya akili mnamo 1990.

Vipi kuhusu matibabu yaliyokusudiwa kubadili mwelekeo wa mapenzi ya jinsia moja kwenda mapenzi ya jinsia tofauti?

Kuwa msagaji, shoga, au mpenda jinsia mbili ni kawaida kabisa na ni afya. Mapenzi ya jinsia moja na ya jinsia tofauti si magonjwa na hivyo hayahitaji matibabu. Hadi leo, hakuna utafiti wa kutosha wa kisayansi kuonyesha kwamba tiba inayolenga kubadili mwelekeo wa mapenzi ya jinsia moja ni salama au inafaa. Kwa kuongezea, inaonekana kwamba uhamasishaji wa matibabu ya mabadiliko huimarisha ubaguzi na huchangia mazingira mabaya kwa wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili.

Ushoga ni jambo la Magharibi, au “lisilo la Kiafrika”?

Hapana. Ushoga umekuwa sehemu ya kila jamii na kila tamaduni, na pia hutokea kwa wanyama. Tafiti tofauti kote ulimwenguni zimegundua kuwa kati ya mtu mmoja hadi kumi kati ya 100 wanavutiwa na wahusika wa jinsia moja. Moja ya dhihirisho la mapema zaidi ulimwenguni la ushoga ni michoro ya miamba ya watu wa San Zimbabwe ambayo inaonyesha mahususiano ya jinsia moja ambalo ni la maelfu ya miaka iliyopita. Michoro hiyo na vile vile ushahidi mwingine wa kihistoria unaonyesha kuwa ushoga umekuwepo katika bara lote la Afrika katika historia yote, na sio umeletwa na mataifa ya Magharibi kama inavyodaiwa na viongozi wa kiafrika na watu wengine.

Jamii au dini zinaweza kuhalalisha ubaguzi?

Tamaduni za kijamii au za kidini haziwezi kuhalalisha tena ubaguzi dhidi ya watu walio wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili kwani tamaduni za namna hii zinaweza kuhalalisha ubaguzi wa rangi na kijinsia. Uonevu na unyanyasaji, kuwakatalia watu walio wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili fursa sawa na heshima au kuwatuhumu kwa vile walivyo sio uchaji wa Mungu wala ufuataji tamaduni bali ni ubaya.

“Kutoka nje” (“coming out”) ni nini na kwa nini ni muhimu?

Kuwaambia watu wengine kuwa wewe ni mpenzi wa jinsia moja au tofauti huitwa “kutoka nje.” Kutoka nje mara nyingi ni hatua muhimu ya kisaikolojia kwa watu walio wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili. Wanawake wasagaji na wanaume mashoga ambao wanahisi lazima wafiche mielekeo yao ya kimapenzi huripoti wasiwasi wa mara kwa mara wa afya ya akili kuliko wanawake wasagaji na wanaume mashoga ambao wako wazi. Japokuwa, unapaswa kutoka nje tu ikiwa unataka, na ikiwa uko tayari. Ingawa unatumaini kuwa marafiki na familia watakuunga mkono, inawezekana kwamba hawatakubali. Ikiwa unategemea wazazi wako kifedha, unaweza kutaka kungojea. Inawezekana kwamba wanaweza kuguswa vibaya na kujaribu kukufukuza nyumbani, kukuweka kwenye ndoa ya jinsia tofauti au kwenye matibabu mabaya ya kiakili na yasiyo muhimu. Kama utatoka nje, ni wazo zuri kuanza kwa kumwambia mtu ambaye una uhakika kuwa atakuwa na mtizamo mzuri. Kutoka nje kunaweza kuwa moja ya kazi ngumu sana utayokabiliana nayo katika maisha yako, lakini pia inaweza kuwa moja ya kazi zenye tunu sana. Kutoka nje ni njia moja ya kudhibitisha hadhi yako na hadhi ya watu wengine walio wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili.

Je ushoga ni dhambi?

Uyahudi, Ukristo, na Uislam kitamaduni huchukulia tabia za mapenzi ya jinsia moja kuwa ni dhambi. Mafundisho ya Uhindu, Wabudha, Jain, na Sikh hayako wazi kabisa juu ya mwelekeo wa mapenzi ya jinsia moja, na viongozi wa dini wanatoa maoni tofauti. Leo, viongozi kutoka dini zote wanazidi kukubali mapenzi ya jinsia moja, na baadhi yao huenda mbali hadi kuhimiza ndoa ya jinsia moja. Wanazuoni wa Kislamu, kwa mfano, wanasema kwamba Uislam haulaani ushoga na kusema kwamba, wakati Kurani inazungumza dhidi ya tamaa ya ushoga, iko kimya juu ya mapenzi ya jinsia moja. Papa Francis, mkuu wa Kanisa Katoliki, ameongea mara kwa mara juu ya hitaji la Kanisa Katoliki kuwakaribisha na kupenda watu wote, bila kujali mwelekeo wao wa kimapenzi, na kuweka wazi kuwa mafundisho ya Kikatoliki yanasema kwamba tabia za ushoga “sio dhambi.” Idadi inayokua ya makanisa ya Kikristo hufanya baraka za ndoa za jinsia moja. Watu wengi walio wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili barani Afrika, pamoja na wafuasi wa dini zote, wanaripoti kwamba hawapati mzozo kati ya mwelekeo wao wa kimapenzi na imani yao.

Kwa kifupi:

Ni sawa kuwa msagaji, shoga, au mpenda jinsia mbili, na ni asili kama kuwa mpenzi wa jinsia tofauti. Kuwa msagaji, shoga, au mpenda jinsia mbili sio ugonjwa, shida ya akili au ulemavu; ni kawaida kabisa na ni afya, kama ilivyo utofauti wa binadamu, kutumia mkono wa kushoto.

Kama wewe ni msagaji, shoga, au mpenda jinsia mbili, hauko peke yako. Kuna mamilioni ya wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili barani Afrika. Wengi wao wamewekwa katika vikundi ambavyo unaweza kupata msaada.

Haki za mashoga ni haki za binadamu. Sheria zinazofanya mapenzi ya jinsia moja kuwa uhalifu zinapingana na kanuni za msingi za haki na usawa, na zinakiuka sheria za haki za binadamu za kimataifa. Zinaimarisha unyanyapaa wa kijamii, zinahimiza ubaguzi usio sahihi, zinadhoofisha juhudi za afya ya jamii, na hazilengi chochote isipokuwa ubaguzi.

Unaweza kusaidia kupunguza ubaguzi, unyanyapaa, na ukatili dhidi ya watu wasagaji, mashoga, na wapenda jinsia mbili kupitia utetezi na uhamasishaji.

Kumbuka: Mtu yeyote anaweza, bila kuomba ruhusa, kuzalisha maandishi haya kwa matumizi yasiyo ya kibiashara na ya kielimu. Sehemu za haya maandishi ni tafsiri ya vijisehemu kutoka kwenye tovuti ya Jumuiya ya Kisaikolojia ya Marekani (APA). Maandishi asilia yanaweza kupatikana www.apa.org/topics/lgbt/orientation.pdf