Mahojiano: WanaLGBT Tanzania

🇺🇸 Please click here to find an English version of this interview.

Wasagaji, mashoga, wapenda jinsia mbili na wabadilisha jinsia (LGBT) wanakumbwa na ubaguzi na vurugu ambazo zimesababisha madhara makubwa pamoja na ubinywaji wa haki zao za msingi. Niliwahoji wanaharakati watatu wa LGBT wa Tanzania ambao ni wanachama wa jamii hii ili kujua zaidi kuihusu. Lulu ni msagaji mwenye zaidi ya miaka ishirini, Grace ni mwanamke aliyebadilisha jinsia mwenye umri wa kati ya miaka ishirini na Baraka ni shoga mwenye umri wa miaka thelathini na nusu. Haya sio majina yao halisi, maana wanaishi Tanzania na hawahisi salama kujitokeza hadharani. Wanayopitia ni ya kuhuzunisha kwakweli. Nawashukuru kwa kuwa na ujasiri wa kuhojiwa. Natumaini kusoma kuhusu gharama ya maovu ya chuki dhidi ya wapendao jinsia moja na wabadilisha jinsia itamsaidia msomaji kuelewa umuhimu wa kupigania haki za wanaLGBT nchini Tanzania.


Faharasa

Mwelekeo wa kimapenzi (sexual orientation) — Muundo wa kudumu wa mvuto wa kihemko, wa kimapezi au wa kijinsia.
Upenda jinsia tofauti (heterosexuality) — Mvuto wa kihemko, kimapenzi au kijinsia wa jinsia tofauti.
Ushoga (homosexuality) — Mvuto wa kihemko, kimapenzi au kijinsia wa jinsia moja.
Wanawake wasagaji (lesbian women) — Wanawake wanaovutiwa na wanawake wenzao kihemko, kijinsia au kimapezi.
Wanaume mashoga (gay men) — Wanaume wanaovutiwa na wanaume wenzao kihemko, kijinsia au kimapenzi.
Upenda jinsia mbili (bisexuality) — Upendo au mvuto wa kimapezi ama kihemko wa jinsia zote mbili.
Chuki dhidi ya mashoga (homophobia) — Woga, chuki na ubaguzi dhidi ya watu wapendao jinsia moja.
Jinsia (sex) — Utambulisho wa jinsia ambao mtu alizaliwa nao.
Utambulisho wa jinsia (gender identity) — Utambulisho wa jinsia ambao mtu binafsi hihisi. Unaweza kuwa wa kike, kiume ama mwingine. Unaweza kuwa sawa ama tofauti na wa kuzaliwa.
Wabadili jinsia (transgender) — Mtu ambaye utambulisho wa jinsia yake haulingani na aliozaliwa nao. Anaweza kuwa mpenda jinsia tofauti, shoga, msagaji ama mpenda jinsia mbili.
Mwanamke aliyebadili jinsia (trans woman) — Mwanamke aliyezaliwa kama mwanamme.
Mwanamme aliyebadili jinsia (trans man) — Mwanamme aliyezaliwa kama mwanamke.
Chuki dhidi ya waliobadili jinsia (transphobia) — Woga, chuki au ubaguzi dhidi ya waliobadili jinsia.
Wasagaji, mashoga, wapenda jinsia mbili na wabadilisha jinsia (LGBT) — Wanawake wapendao wanawake wenzao kimapezi, wanaume wapendao wanaume wenzao kimapenzi, wanaopenda jinsia mbili na wabadilisha jinsia.
Kujitokeza (coming out) — Kukubali na kutangaza mwelekeo wa kijinsia kwa umma.
Kumtokeza mwananachama wa jamii ya LGBT bila ruhusa yake (outing) — Kutangaza mwelekeo ama utambulisho wa jinsia wa mwanaLGBT bila ruhusa yake.


Je ni katika umri gani na namna gani uligundua kuwa wewe ni mwanaLGBT?

Lulu: Nilikua najua kuwa nilivutiwa na wasichana lakini sikuweza kudhihirisha hisia zangu hadi nilipofikisha umri wa miaka kumi na nane ilipokuwa vigumu kuziepuka. Nilivutiwa na binti tuliyeishi kwenye eneo moja. Nilijaribu sana kuepuka hiyo hisia lakini ilizidi. Ilinibidi nikubali hizo hisia maana kuziepuka kulisababisha mfadhaiko na msongo wa mawazo. Sikufanya lolote kuhusu hisia zangu lakini niliamua kujifunza na kuelewa zaidi kuhusu mambo ya (LGBT). Ilinichukua miaka mitatu kutoka kwenye dhiki na kuchukua hatua ya kwanza kukubali kuwa mimi ni msagaji.

Grace: Niligundua kwamba nilivutiwa na wanaume wakati nilipomaliza shule ya sekondari, nilipokuwa na umri kati ya miaka 15 au 16. Nilianza kuvaa nguo za wasichana na nywele bandia kisiri. Nilijipata mwenyewe nikiyapenda mambo ya wasichana zaidi. Kwa kuwa nilivutiwa na wanaume, nilidhani mimi ni shoga. Ni baada ya miaka mitatu nilipojua mimi ni mwanamke mpenda jinsia tofauti aliyebadili jinsia.

Baraka: Niligundua kuwa mimi ni shoga nikiwa na umri wa miaka kumi na minne tu.

Je hali yako ya kuwa mwanaLGBT unaishi nayo vipi au inapokelewaje nchini Tanzania?

Lulu: Ni ngumu sana. Ubaguzi uko juu sana. Ni lazima nijifanye kuwa mimi ni mpenda jinsia tofauti kwani naogopa kwamba, kama watu watajua, wanaweza kuniumiza kihisia ama kimwili. Ni lazima nichague eneo la kuishi kwa kuwa naweza fukuzwa na majirani wakihisi mimi ni msagaji. Naishi nikijua siku moja familia yangu itanioza kwa mwanaume. Najiandaa kukataliwa na familia yangu. Ni ngumu lakini tunajaribu sana kuungana mikono sisi kama wanaLGBT na tunashirikiana kama familia. Mahusiano ya kimapenzi ni ngumu zaidi kwa kuwa wasagaji wengi wameolewa na wanaume na huwa na mwanamke mpenzi kama nyumba ndogo. Jambo hili husababisha ugomvi na mabwana zao wakijua wanaripoti kwa familia zetu. Tunaishi kwa uwoga wa kufutwa kazi kwa sababu tu ya kupenda mtu wa jinsia moja.

Grace: Imekuwa vigumu sana kwa sababu ya mila na desturi zetu. Inachukuliwa kama laana, ndio maana nilijaribu kuweka jambo hili siri hata kwa jamii yangu lakini siku moja picha ambazo nilikaa msichana zilisambaa mtandaoni. Watu wengine wanasema kuwa mimi ndiye chanzo cha Coronavirus. Familia yangu ilinikataa walipojua na hawakuniongelesha tena hadi leo. Woga ulifanya nihame na sasa najaribu kujenga maisha mapya ambayo ni magumu.

Baraka: Kwa kiasi kikubwa inachukuliwa vibaya na ninaonekana kuwa mtu nisie na maana mbele ya jamii japokuwa kuna watu wachache ambao wanaichukulia ni kama hali ya kawaida na wananiheshimu na kunithamini pia.

Je familia yako inajua kuwa wewe ni mwanaLGBT? Je Marafiki zako wanajua wewe ni mwanaLGBT? Ikiwa rafiki zako na familia yako wanajua hivyo, je uliwajulishaje kwamba wewe ni mwanaLGBT? Mwanzoni walipokea vipi taarifa ya wewe kuwa ni mwanaLGBT? Je walikuunga na wanakuunga mkono? Ikiwa hujaiambia familia yako, uhofu ya kitu gani kikubwa kitatokee iwapo utawaambia?

Lulu: Familia yangu ilishuku kuwa mimi ni msagaji nikiwa katika chuo kikuu. Waliacha kunipa pesa zozote na hawakuongea nami tena. Walinilaumu kwa mambo yote mabaya yaliyotendeka. Hata nilipomaliza chuo kikuu na kukosa kazi walisema sababu ni kwamba mimi ni msagaji na nimelaaniwa. Walisema nitakufa maskini. Walisema wanajuta kulipa karo yangu. Walinikubali nilipopata kazi kwa sababu naweza kujimudu na kuwamudu pia. Nasikitika kwamba wakati nitashindwa kuwamudu watanikataa tena. Marafiki wangu wote ni wasagaji mbali na wawili tu ambao huniunga mkono na kunipenda.

Grace: Baada ya watu kutangaza kuwa mimi ni mbadili jinsia niliachwa na kubaki na marafiki wachache wanaoendelea kuniunga mkono. Wengi niliodhani ni marafiki walinikataa kabisa na kuanza kuninyanyasa.

Baraka: Familia yangu yote na marafiki wanajua kuwa mimi ni shoga. Familia ilijua waliposikia kutoka kwa jamii iliyokuwa inaishi jirani na maeneo tuliokuwa tunaishi kutokana na matendo yangu ambayo mengi yalikuwa ni ya kike. Waliniuliza nakumbuka ilikuwa mwaka 2000 na niliwajibu kuwa mie ndio ni shoga. Iliwashtua na ilikuwa ngumu kupokea. Ilibidi nifukuzwe nyumbani na mpaka sasa sikuwahi kurudi nyumbani japo nipo na mahusiano mazuri na baadhi ya wana familia.

Je wewe ni muumini wa dini? Ikiwa ndivyo, unawezaje kupatanisha utambulisho wako kama mwanaLGBT na imani yako?

Lulu: Nililelewa katika Ukristo. Namwamini Mungu na Yesu. Naamini kuwa Mungu hatuchukii lakini binadamu wanatumia dini kutufanya tuonekane kama wenye dhambi. Lakini najua kuwa upendo hauwezi kuwa dhambi kamwe.

Grace: Mimi ni Mkatoliki ninayemwamini Mungu. Nafuata dini sana. Ninapoenda kanisani, navaa nguo za kiume na kuvaa nguo za kike ninaporudi nyumbani. Najua kwamba Mungu yupo nyuma yangu na atalinilinda daima. Kwake yeye, utambulisho wangu haumjalishi. Aliniumba nikiwa mwanamme aliyebadili jinsia na ananipenda nilivyo.

Baraka: Mimi sio muumini japokuwa naamini Mungu.

Je unaweza kuelezea aina tofauti za ubaguzi ambao wanaLGBT wanakabiliana nao nchini Tanzania? Je tofauti zipo katika huduma za afya, elimu, na ajira?

Lulu: Watoa huduma za afya hutuuliza maswali yenye hukumu ambayo hutufanya tuhisi vibaya. Shuleni, wanaposhuku kuwa mtu si mpenda jinsia moja wanamfukuza. Tunafutwa kazini pia.

Grace: Tunapata shida na wenye nyumba na ni ngumu kwetu kupata nyumba za kuishi. Tunanyanyaswa kwenye mtandao na kutengwa na jamii.

Baraka: Watu wenye mahusiano ya jinsia moja wanakabiliana na ubaguzi katika viwango tofauti, kwenye huduma za afya mara nyingi kumekuwa na unyanyapaa wa kimatendo na hata wa kimaneno dhidi ya mashoga, kwenye ajira mashoga wengi wamekuwa wakipata ugumu kupata nafasi za ajira pia hata muda mwingine wamekuwa wakifukuzwa kazi kutokana na jinsi walivyo au muda mwingine kutokana na mitazamo hasi iliyo katika jamii dhidi yao, upande wa elimu pia zipo changamoto kama za kutengwa na kuongelewa maneno mabaya na muda mwingine kuundiwa njama za kukuchafua ili ufukuzwe shule/chuo.

Je ni jinsi gani hali ya usagaji kwa wanawake inatofautiana na hali ya ushoga wa wanaume nchini Tanzania?

Lulu: Wanawake wasagaji wanalazimishwa kuolewa na kubakwa. Hivyo ndivyo familia zetu hukumbana na hali hii wanapogundua kwamba sisi si wapenda jinsia tofauti.

Grace: Nadhani wanawake mashoga wanakubalika kidogo kuliko wanaume sababu ni sawa kwa mwanamke kuwa na tabia za kiume lakini si sawa kwa wanaume kuwa natabia za kike.

Baraka: Hali ya usagaji ni tofauti ukilinganisha na ushoga kwa sababu wasagaji wengi kuwa katika mionekano ya kike tofauti na mashoga ambao wengi wao wanamionekano ya kiume hivyo huwapelekea kujulikana mapema kuwa ni mashoga pale wanapoonyesha tabia tofauti na wanaume wengine.

Je umewahi kufikiria kuondoka nchini kwa sababu ya ubaguzi unaowakabili wanaLGBT au ubaguzi wowote uliokutana nao?

Lulu: Ndio. Mara nyingi haswa viongozi wa kisiasa wanapotoa hotuba za chuki kuhusu jamii ya wanaLGBT.

Grace: Ndio. Nimekuwa nikifikiria kutafuta kimbilio nje ya nchi kwa kuwa niko peke yangu humu na siwezi kuwa mimi mwenyewe.

Baraka: Nilishawahi kutaka kufanya hivyo kipindi cha miaka kumi iliyopita lakini baadaye niliachana na huo mpango.

Je unafikiri maisha yako ya mbeleni yatakuwaje?

Lulu: Naona siku za usoni zenye kung’aa. Najua nitapitia changamoto nyingi kwa sababu mazingira si ya kirafiki. Nafanya kazi kwa bidii ili niweze kujisimamia. Ni lazima niwe na utulivu wa kifedha ili niishi.

Grace: Sioni siku za usoni humu Tanzania. Kama ninazo, ni nje ya nchi. Tunachokitarajia humu ni kifo tu.

Baraka: Yatakuwa mazuri kutokana na namna ya aina ya maisha ninayoishi na mipango mizuri niliyojiwekea.

Athari ya unyanyapaa katika huduma za afya na ustawi wao ni mbaya sana kwa wanaLGBT. Hivyo, inasemekana, kiwango cha majaribio ya wanaLGBT kujiua kipo juu kutokana na kutengwa, unyanyasaji na uonevu. Je! Una ushauri wowote kwa wanaLGBT wa kiume au wakike?

Lulu: Ushauri ninaoweza kuwapa ni kusimama imara kama msemo wa Kiswahili usemao “hakuna marefu yasiyo na ncha.” Wanafaa kutia bidii ili kujisiamamia kifedha. Unapokuwa na uwezo wa kifedha, utaepukana na mambo mengi. Pia simamia imani yako, jua haki zako na kukabiliana na watu wanapokiuka haki zako. La muhimu zaidi ni kujikubali mwenyewe na kujipenda mwenyewe zaidi.

Grace: Usijitokeze kwa mtu yoyote! Hujui nani atakugeukia. Lazima ufikirie matokeo ya kujitokeza. Shauri langu ni: jikaze kimasomo ili uhitimu na upate kazi nzuri. Unapojisimamia unapata uhuru na nguvu.

Baraka: Ushauri wangu ni kwamba kuwa shoga sio mzigo au laana hivyo pindi wanapopatwa na changamoto hizo wajaribu kutafuta njia za kuzitatua. Kuna mashirika na baadhi ya watu ambao wapo katika jamii wanaoweza kuwasaidia na pia kutatua hizo changamoto.

Uchunguzi wa kimataifa uliofanywa na kituo cha utafiti cha Pew mnamo 2007 uligundua kwamba asilimia 3 tu ya watanzania wanaamini kuwa ushoga unapaswa kukubaliwa nchini. Hiki ni kiwango cha chini kabisa katika nchi zote zilizochunguzwa. Je! Kwanini unafikiri ushoga unakubalika kwa kiwango kidogo Tanzania ukilinganisha na nchi zingine ambazo zinapingana na zenye sheria za kuhukumu ushoga?

Lulu: Watanzania wana maarifa madogo kuhusu wanaLGBT. Wanaamini kuwa wazungu ndio waliyaleta. Wanaamini kuwa kupenda jinsia tofauti ndio sahihi tu na hawapo tayari kujifunza. Watu wengine wa jamii ya LGBT wanajichukia na kuchukia wenzao pia.

Grace: Sababu kuu ni mila na tamaduni. Kuna unafiki mwingi. Wasemao tumelaaniwa wanataka kushiriki ngono nasi usiku. Kuna msemo usemao “aliyelaaniwa mchana na kubarikiwa usiku.”

Baraka: Sababu kubwa ni imani za kidini, mila na maadili zilizoota mizizi katika akili na mioyo ya jamii. Hizo ndizo zinazopelekea kuwepo na kiwango hicho kidogo.

Ni nini kinachohitajika kufanyika ili kubadilisha mitazamo hasi juu ya ushoga nchini Tanzani?

Lulu: Tunahitaji mafunzo kwenye familia kuhusu mambo haya ya LGBT. Watu wenye ushawishi wanafaa kuongelea mambo haya ya LGBT kwa njia chanya.

Grace: Watu wanafaa kufunzwa kuhusu mambo haya. Tunataka kukubaliwa. Tunataka watu waelewe kuwa hakuna haki za mashoga ila tu haki za binadamu. Tunafaa kufanya kampeni. Tunafaa kuwaongelesha wazazi na jamii. Watu wanafaa kujua tupo na tupo hapa kukaa. Tunahitaji kuungwa mkono hadi na nchi za nje.

Baraka: Tunahitaji jamii inayojenga ufahamu kuhusu maswala ya LGBT ili kusaidia kubadilisha mitazamo hasi dhidi ya mashoga nchini.

Je! Vyombo vya habari vinasababisha au kuchangia vipi kutangaza au kukuza maoni hasi yanayopinga wanaLGBT nchini Tanzania?

Lulu: Vyombo vya habari vinatumia lugha yenye chuki na huleta habari kwa njia inayoonyesha kuwa ushoga ni dhambi na tabia mbaya.

Grace: Vyombo vya habari humu Tanzania huchapisha habari za uwongo kuhusu wanaLGBT ambazo huendeleza aina ya ubaguzi. Habari kuhusu wanaLGBT huwa hasi si chanya. Wanahabari hawataki kufanya kazi ya kutujua vizuri ili watuelewe. Wanaogopa serikali pia kwa sababu inapinga haki za wanaLGBT. Habari chanya kuhusu wanaLGBT yaweza waletea wanahabari shida kubwa na serikali.

Baraka: Kwanza kabisa wengi wa watu wanaofanya kazi katika vyombo vingi vya habari ni sehemu ya jamii kubwa yenye mtazamo hasi dhidi ya ushoga ndio hicho kinapelekea vyombo vya habari kuendelea kuchochea chuki au mitazamo hasi dhidi ya mashoga nchini.

Ndani ya Tanzania Bara, ni haramu kwa wanaume kufanya ngono na wanaume wenzao, na vitendo hivyo, hubeba adhabu ya kifungo cha maisha, wakati vitendo vya ngono kati ya wanawake havizuiliwa kabisa. Huko Zanzibar, vitendo vya ngono kati ya wanawake kwa wanawake vinaadhibiwa kwa kifungo cha miaka mitano, na vitendo vya ngono kati ya wanaume kwa wanaume ni kifungo cha hadi miaka 14. Je! Sheria hizi zinaathirije maisha ya kila siku ya wanaLGBT nchini Tanzania?

Lulu: Tunaishi kwa woga kuwa ipo siku tutapelekwa mahakamani. Mara nyingine tunajihisi kama wahalifu. Hatuna uhuru.

Grace: Sheria inatumiwa kuwatisha jamii ya LGBT pamoja na polisi. Watu watakutisha na kuchukuwa mali yako kama simu na vitu vingine vyenye thamani. Sheria inatufanya tuogope kuripoti unyanyasaji wowote kwa polisi maana hatutarajii usaidizi wowote.

Baraka: Kukosekana kwa tafsiri sahihi juu ya sheria zinazosemekana zinapinga au kukemea ushoga na usagaji, kumesababisha mashoga wengi na wasagaji kudhulumiwa haki zao za msingi za kibinadamu, na kuishi maisha ya tabu yaliyojaa vitendo vya uonevu na ukatili.

Katika kesi muhimu juu ya ushoga kwa Afrika ni ile ambayo Botswana waliruhusu ngono kwa mashoga. Je! Hii inamaanisha nini kwa nchi zingine za Kiafrika? Je! Ni wakati muhimu sasa kwa watetezi wa haki za binadamu kupambania sheria ambazo zinahalalisha ushoga nchini Tanzania? Na je unadhani au kufikiri sheria za haki kwa mashoga zinaweza kuja kubadilika ndani ya Tanzania hapo baadaye?

Lulu: Hatua ndogo zinaweza saidia. Nadhani tunafaa kuanza kwa kubadilisha akili za watu binafsi. WanaLGBT na wengine wanafaa kuona wapendao jinsia moja kama binadamu wanaofaa haki na heshima kama wapendao jinsia tofauti.

Grace: Wanaharakati wa Botswana wamefanya kazi kwa bidii ili kuwezesha haya. Napenda kazi yao na inanitia msukumo. Utakuwa mchakato mrefu na mgumu kukubali ushoga Tanzania lakini maendeleo katika maeneo mengine Afrika yanatupa moyo na motisha.

Baraka: Jamii kubwa ya kiafrika bado ipo na mtazamo hasi dhidi ya ushoga kutokana na sababu za kiimani na tamaduni hivyo wengi hawakufurahishwa na uamuzi uliofikiwa na Botswana. Ni muhimu watetezi wa haki za binadamu wakaendelea kupaza sauti zao dhidi ya sheria hizo zilizopitwa na wakati zinazochochea vitendo vya dhuluma dhidi ya mashoga, Pia naamini ndani ya miaka hamsini hadi mia ijayo Tanzania nayo itakuja kubadilisha sheria hizo na kuruhusu mashoga kuishi maisha huru.

Chini ya uongozi wa Rais Magufuli, serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya harakati za kupingana vikali na mahusiano ya jinsia moja. Kampeni hii ilianza mnamo 2016, kupitia Wizara ya Afya ambayo ilisitisha mipango ya kuzuia VVU/UKIMWI ambayo ilikuwa imeundwa kwa ajili ya mashoga. Hapo hapo, Waziri, Hamisi Kigwangalla, alituhumu mashirika ya afya kwa “kukuza ushoga.” Tangu wakati huo, wanasheria na wanaharakati wa haki za binadamu wamekamatwa kwa kufanya semina juu ya haki za wanaLGBT. Pia, Paul Makonda, mkuu wa mkoa wa awali wa Dar es Salaam, ametishia “kuwinda” wanaume mashoga katika mji wake. Je! Yote haya yameathiri vipi afya na ustawi wa wanaLGBT nchini Tanzania?

Lulu: Athari za hayo matendo kutoka kwa wanasiasa zinabaki kwa muda mrefu. Hizo kauli zinaipa jamii nguvu ya kuwabagua na kuwanyanyasa mashoga na wasagaji. Watu wanafukuzwa kutoka manyumba wanayokodisha na makwao na inakuwa ngumu sana kupata huduma za kiafya. WanaLGBT walio na VVU wanawachwa bila dawa.

Grace: Watu wanatumia kauli za wanasiasa zenye chuki kwa wanaLGBT kutunyanyasa na kutupiga bila kujali. Tunaambiwa, “Usiponipa pesa nitakuripoti kwa polisi ama kuweka picha yako kwa mtandao.” Wahalifu wanapewa nguvu na walio na cheo kama raisi na kamishna wa mkoa.

Baraka: Mkakati wowote ambao umefanywa na serikali ya awamu hii ya tano dhidi ya ushoga nchini umeleta madhara makubwa sana kwa mashoga na wasagaji maana wengi wamepoteza maisha iwe kwa kukatiza uhai wao wenyewe kwa kushindwa kuvumila dhulma na manyanyaso dhidi yao, wapo waliooacha kutumia dawa za kufubaza makali ya VVU, wapo waliopata matatizo ya afya ya akili, na wengine kupelekea kujiingiza katika matumizi mabaya ya vileo.

Ni nini kilikuchochea na kukufanya kushiriki katika harakati za haki za wanaLGBT nchini Tanzania? Je! hali ya harakati za sasa ikoje?

Lulu: Nilihisi kuwa mabadiliko niliyotaka hayangetendeka hivyo tu. Lazima niwe kati ya wanaharakati ili kusababisha mabadiliko. Harakati inaenda polepole baada ya ubishi, kwa woga wa kukamatwa ama kunyarwa na watu wasiojulikana. Lakini tunajaribu jinsi tuwezavyo kuwaunga wanaLGBT pamoja na kutoa shauri na uhamasishaji.

Grace: Kuna mashirika kadhaa inayofanya kazi ili kuendeleza haki za wanaLGBT humu Tanzania. Wanazingatia ujenzi wa utetezi na ufahamu katika jamii zetu. Wako na semina za wanaLGBT ambazo wanafunzwa kujihusu, usalama wa cyber na jinsi ya kukabiliana na unyanyasaji. Kipengele kingine cha muhimu katika uharakati ni vipindi vya ushauri kwa familia za wanaLGBT ili kuwasaidia kuelewa kuwa hakuna kitu kibaya na wana wao wasagaji na mashoga na wanafaa kuwakubali na kuwaunga mikono. Tunajaribu kuendeleza haya mambo lakini tunauhofia usalama wetu. Kinachotuweka motisha ni tumaini kuwa tutaona matunda ya bidii yetu.

Baraka: Ni baada ya kupitia changamoto za unyanyapaa, kutengwa, vitendo vya uonevu na ukatili kama kupigwa na jamii yenye mtazamo hasi juu ya ushoga pia manyanyaso na usumbufu kutoka kwa polisi.

Je! Una hofu juu ya usalama wako binafsi kwa sababu ya harakati zako?

Lulu: Kila wakati. Nimechukua mafunzo ya usalama kwa hivyo mimi hurekodi jambo lolote linalotishia usalama wangu na kujaribu kuepuka hatari.

Grace: Ninaelewa hatari ya usalama wangu kabisa unaosababishwa na uharakati wangu. Wanaharakati wengine wa haki za mashoga walikamatwa na wengine kukosekana. Tunajaribu kujihadhari kwa kutokutana na watu tusiowajua na kuwasiliana nao kwenye mitandao tu lakini tunaelewa kuwa mwanaharakati ni hatari.

Baraka: Huwa nina hofu sana na ulinzi na usalama wangu kutokana na mambo yaliyowatendekea wanaharakati wengine nchini.

Je! Kwanini watanzania ambao sio wa jamii ya LGBT wajali juu ya haki za wanaLGBT?

Lulu: Kwa sababu sisi wote ni binadamu. Sisi si tofauti na wao. Tunapenda tofauti na wao. Tunaposema kuwa Tanzania ni ya umoja sisi tumo kati ya huo umoja. Tunalipa ushuru kama wao na tunajenga nchi kama wao. Sisi si wahalifu.

Grace: Kwa sababu hawajui tunayokumbana nayo. Wangalijua, wangalituhurumia. Wangetembea kwa viatu zetu kwa dakika kidogo na kupitia ubaguzi na vurugu tunazopitia sidhani wangevumilia.

Je! Unajibu nini kwa watu wanaosema kwamba ushoga “sio-uafrika” au unaenda kinyume na tamaduni za kitanzania?

Lulu: Mimi ni mfano mzuri wa usagaji Afrika kwa kuwa niliwapenda wanawake kabla nijue kuwa kuna usagaji Marekani na Ulaya. Mwelekeo wa kimapenzi hauhusiani vyovyote na dini, utamaduni ama bara. Upendo ni upendo. Unatokana na mtu binafsi.

Grace: Huo ni uwongo. Tuliumbwa na Mungu mmoja. Na jinsi mtu alivyo ndivyo Mungu alikusudia. Ni kama tulivyo na watu walio na ualbino na ufupi kila mahali na wamo katika mpango wa Mungu. Sisi wote ni uumbaji wa Mungu.

Baraka: Mimi huwajibu kuwa ushoga ni Baraka na si dhambi kwa sababu naweza fanya lolote yeyote anaweza kufanya hadi kuwa raisi.

Asante kwa kuchukua muda wako kuongea name.

Kujua zaidi kuhusu maswala ya ushoga bonyeza hapa. Bofya hapa kujifunza zaidi kuhusu jinsia. Ripoti kuhusu ubaguzi wa serikali dhidi ya wanaLGBT Tanzania na mashirika ya Human Rights Watch na Human Dignity Trust zinaweza kupatikana hapa na hapa.

Picha na tafsiri: Njeri Kinuthia