
Namna tunavyowatendea wanyama inaonyesha kwa kiasi kikubwa utu wetu. Wanyama hawawezi kuzungumza lugha zetu, lakini wana uwezo wa kuhisi. Wanahisi maumivu, hofu, furaha na faraja—kama sisi. Wanathamini maisha yao, kama sisi tunavyothamini yetu.
Hata hivyo, kila siku wanyama wengi wanateseka. Katika mashamba, maabara, na shughuli za burudani mbalimbali, mara nyingi wanachukuliwa kama vitu tu—vitu vya kutumiwa, kudhibitiwa au kutupwa.
Ni kwa sababu hii kwamba tumeanzisha Sio Kitu.
Tulichagua jina hili kuwasilisha wazo rahisi lakini lenye nguvu: wanyama si vitu. Ni nafsi—viumbe wenye maisha yao, uzoefu wao, na mtazamo wao wa dunia. Kama wewe na mimi, wao pia wanaishi kwa namna ambayo ina umuhimu kwao. Kutambua hili ni hatua ya kwanza kuelekea kuwaheshimu ipasavyo.
Kwa sasa, taarifa nyingi kuhusu maadili ya namna tunavyowatendea wanyama zinapatikana zaidi katika lugha nyingine, na kwa Kiswahili bado ni chache. Kupitia Sio Kitu, tunataka kuunda nafasi ya mazungumzo kuhusu haki za wanyama kwa Kiswahili—mazungumzo yanayozingatia hasa falsafa ya haki za wanyama.
Ninaendesha mradi huu pamoja na wanafalsafa wenzangu wawili, Wilson John Simon na Subira Ndutu, ambao nimewafahamu kwa miaka mingi. Wote wawili walikuwa wanafunzi wangu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Wilson pia alikuwa mtu wa kwanza nchini Tanzania kuandika tasnifu ya Shahada ya Uzamili kuhusu mada katika maadili ya wanyama, chini ya usimamizi wangu. Historia yetu ya pamoja kitaaluma na ushirikiano wetu wa muda mrefu ndiyo msingi wa mradi huu.
Kwa pamoja, tunalenga kuchunguza kwa kina maswali muhimu kama vile: Tunawajibika kwa kiwango gani kwa wanyama? Je, wanyama wana haki? Na ikiwa wana haki, haki hizo zinapaswa kuheshimiwa vipi katika maisha yetu ya kila siku?
Lengo letu si tu kushiriki taarifa, bali pia kuchochea tafakari ya kina. Tutajadili hoja mbalimbali za kifalsafa, tutachambua mitazamo tofauti, na tutajaribu kujenga mjadala unaoheshimu watu kutoka mazingira na tamaduni mbalimbali.
Iwe unaanza kujifunza kuhusu mada hii au umekuwa ukiifikiria kwa muda mrefu, unakaribishwa kujiunga nasi.
Unaweza kufuatilia Sio Kitu hapa:
- Instagram: instagram.com/haki_za_wanyama
- Facebook: facebook.com/hakizawanyama
Tafadhali shiriki mradi huu na washirikishe wengine wanaoweza kupendezwa nao. Kwa pamoja, tunaweza kuanza kujenga uelewa mpana zaidi na kuchukua hatua kidogo kidogo kuelekea dunia yenye huruma na haki zaidi—kwa binadamu na wanyama pia.
Karibu sana.