Mapenzi ya kadi za posta

Kabla ya Facebook na Instagram, kulikuwa na kadi ya posta. Vijana miongoni mwetu huenda hawajawahi kutuma hata moja kwa mtu yeyote yule. Mawasiliano leo hii ni ya haraka, na barua huitwa kwa dharau “barua ya konokono” na umati wa kidijiti. Tokea kadi posta ya kwanza ya picha itumwe kwa mwandishi wa London-Theodore Hook mnamo mwaka 1840, barua ya posta imepata umaarufu kama njia ya kutumiana picha na kushirikiana kimawazo katika maeneo na tamaduni mbalimbali. Katika siku za hivi karibuni, umaarufu huo umepungua sana, kwa sababu ya simu za rununu na mitandao ya kijamii. Kutuma kadi za posta huchukua mda mwingi na nguvu kuliko kutuma barua pepe, au ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, ambayo inafanya kadi za posta ziwe na maana zaidi kuliko ilivyokuwa wakati hakukuwa na njia mbadala ya papo kwa hapo.

Kuandika kadi ya posta kunahitaji utulivu na umakini mkubwa, na kupokea moja huleta hisia binafsi kuliko kupokea ujumbe kwenye kifaa cha kielektroniki. Kadi ya posta inashikika na ni kuponi inayojidhihirisha, na cha ajabu zaidi ni kujua kuwa kipande cha karatasi ulichoshikilia mikononi mwako kilisafiri umbali mrefu na kupitia mikono ya watu wengi ili kukufikishia ujumbe wa mtu mwingine. Wakati “kupenda” (likes) mara nyingi hupewa bila kufikiria sana na kutokupelekea kiwango cha ushiriki wa maana, kuandika barua posta kwa mtu ni zoezi la uvumilivu na uangalifu, na linalodhiirisha kuwa unajali sana.

Mnamo 2005, mapenzi kwa kadi za posta ya mwanafunzi wa wakati huo wa chuo kikuu Paul Magalhães kutoka Ureno zilimfanya kuunda mradi wa Postcrossing. Postcrossing ni jukwaa la mtandao linalowaunganisha watu kutoka kote ulimwenguni. Mbinu ni rahisi: kwa kila kadi posta utakayotuma, utapokea kadi ya posta. Mtu yeyote anaweza kujiunga, bila kujali umri, jinsia, rangi, au imani. Kujiunga na kuwa Postcrosser, unachohitaji kufanya ni kwenda kwa tovuti ya www.postcrossing.com na kuunda akaunti. Mara baada ya kuwa na akaunti, unaweza kuomba kutuma kadi ya posta. Tovuti itakupatia anwani ya bahati nasibu ya mtu usie mfahamu pamoja na namba ya kipekee ya utambulisho ya kadi ya posta. Kisha utatuma kadi ya posta kwa anwani hiyo. Kadiri itakavyokuwa ya kirafiki na ya heshima, unaweza kuandika chochote unachopenda. Unaweza kutuma jambo la kuvutia kutoka sehemu unayoishi, tukio kutoka katika maisha yako, au shairi uliloandika. Kuwa mbunifu! Muhimu, ingawa, lazima ujumuishe namba ya utambulisho ya kadi posta. Mpokeaji wa kadi yako ya posta atatumia namba ya utambulisho kusajili kadi ya posta kwenye tovuti mara tu atakapo ipokea. Halafu utaarifiwa kuwa kadi yako ya posta imefikia, na kisha mtu mwingine atapewa jukumu la kukutumia kadi ya posta.

Hivi sasa, jamii ya Postcrossing ina watu karibu 800,000 wa barua pepe. Hadi sasa wamebadilishana zaidi ya kadi milioni 55, ambazo zimesafiri kilomita 280,683,219,245 kwa pamoja. Kama tovuti inavyosema, hiyo ni “safari 7,003,948 kuzunguka dunia au safari 365,089 kwenda na kurudi mwezini au safari 938 za kwenda na kurudi kwenye jua!” Kila wakati, mamia ya maelfu ya kadi za posta zinasafiri. Kufikia sasa, kadi nyingi za posta zimetumwa kutoka Ujerumani, zaidi ya milioni nane, ikifuatiwa na Urusi na Marekani. Wapenzi zaidi ya 3,000 wa kadi za posta katika Afrika wanaishi Afrika Kusini. 19 tu wanaishi Tanzania. Kwa ujumla, zaidi ya kadi 750 zimetumwa kutoka Tanzania, ikiiweka Tanzania katika kiwango cha 133 kati ya 248 ya jumla ya nchi na mataifa.

Nilizungumza na Watanzania wawili ambao ni Postcrosser juu ya matamanio yao. Wilson, mkulima wa miaka 28 ambaye anaishi Bagamoyo, muhitimu wa ivi karibuni wa shahada ya uzamili katika falsafa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, alijifunza juu ya Postcrossing kutoka kwa rafiki yake wa Ujerumani. Aliamua kujiunga na “kuungana na watu na kujifunza juu ya maisha kutoka sehemu nyingine za dunia,” na kama njia ya kuitangaza nchi yake na tamaduni zake.

Harrison ana umri wa miaka 32 ni fundi wa teknolojia ya habari na anaishi katika jiji la Arusha. Amekuwa akiandika barua tangu utotoni, akianza na barua aliyomwandikia baba yake mwaka 2001, na alifurahi pale aliposikia habari ya kuhusu kadi posta kutoka kwa rafiki yake wa Facebook. Kwake yeye, Postcrossing ni njia ya kupata marafiki wa kalamu. Wote wawili Wilson na Harrison wameambiwa na marafiki kuwa kujihusisha na kadi posta ni kupoteza pesa, ila hilo halijawazuia. Furaha ya kupata kadi ya posta katika sanduku la ofisi ya posta ni nzuri sana na ya thamani kama ilivyo kwa mambo mengine, na hufanya yote ifae kwao.

Postcrossing kunawaleta watu kutoka asili tofauti pamoja, kukuza uelewa wa kitamaduni na urafiki, na huleta tabasamu kwa kila kona ya ulimwengu.


A version of this article was published under the following title:
“Mapenzi kwa kadi za posta yalivyopotea,” Mwananchi (Tanzania, 28 January 2020)