Ubaguzi mubashara: kadhia ya maadili dhidi ya uwepo wa mipaka

Jaalia katika fikra zako kwamba: leo ni siku muruwa ya mwezi wa Septemba. Hakuna joto wala baridi, upepo mwanana unapepea na mawingu yanang’ara angani. Unachukua blanketi lako na kuelekea katika moja ya fukwe huru za jiji la Dar es salaam. Unajiandaa kwenda kujipumzisha ufukweni hapo na kufurahia machweo jua. Bali unapofika ufukweni mipango yako inatibuliwa bila ya kutegemea. Unaelezwa na afisa ulinzi kuwa serikali imeweka sheria mpya za matumizi ya fukwe. Unaambiwa kwamba huwezi kutumia ufukwe huo kwa vile wewe ni mtu mweusi. Watu wengine wowote wanaruhusiwa kutumia fukwe hizo isipokuwa watu weusi tu, na iwapo mtu mweusi yeyote angekaidi amri hiyo basi nguvu ingeweza kutumika.

Hakika, sheria hii mpya inakiuka misingi ya haki kinagaubaga. Inatukumbusha historia ya zile enzi za kiza – ubaguzi wa rangi Afrika Kusini na nyakati za kabla ya vuguvugu za kupigania haki za kiraia kule Marekani. Kutenda ubaguzi kwa misingi ya rangi ni kinyume na haki na maadili kabisa. La kutia moyo ni kwamba ulimwengu unaitambua jinai hii sasa. Kuwa na rangi ya ngozi tofauti, kitu ambacho hakimo katika mamlaka ya mtu, si sababu thabiti wala halali abadan inayomfanya mtu asiweze kuburudika na machweo jua ufukweni katika nchi yake, au kujipatia faida nyingine katika maisha yake eti kwa sababu ya rangi yake.

Je ni sababu gani inayonishurutisha kuzungumzia mada hii ya kawaida mno? Kwa sababu ubaguzi mithili ya huu unafanywa hadharani dhahiri shahiri lakini hautambuliwi kwa uhalisia wake kama ni ubaguzi. Kama vile ambavyo hatuna hiari wala udhibiti juu ya rangi zetu, kadhalika hatuna hiari juu ya uchaguzi wa mahala tuzaliwapo au na kuzaliwa na wazazi gani. Uwepo wa mwanadamu katika ulimwengu huu ni matokeo nasibu tu, waama jambo hili laonekana kuwa moja katika vipengele msingi viamuavyo wapi twaweza kwenda na wapi haturuhusiwi. Endapo wewe ni raia wa Tanzania na ungependelea kuhajiri ili kuishi Ufaransa kwa mintaarafu ya kujitafutia maisha bora, au pengine unapendezwa na hali ya hewa ya huko tu basi Mtanzania huyo itamuwiya vigumu sana kuweza kutekeleza azma yake hiyo. Mtu huyo anaweza kujihatarishia maisha yake kama Waafrika wengi wanavyofanya siku hizi kwa kujiabiri kwenye maboti yanayasafiri kwenye bahari ya Mediterania. Safari hizi za hatari na mashaka makubwa kuelekea Ulaya hazina dhamana, wala hakuna uhakika endapo Mwafrika huyo atakapokanyaga Ulaya hatorudishwa alikotoka na kuizima ndoto yake ya kuishi kwa furaha na amani ughaibuni. Wakati mwingine mtu huyo anaweza kuanza mchakato wa kupata kibali cha kuishi na kufanya kazi pasipo na uhakika wa mafanikio ya ombi lake. Kwa Watanzania wengi suala la kupata viza ya matembezi ni jambo gumu. Bali endapo utakuwa raia wa Ujerumani ama Ugiriki basi mambo yapo tofauti kabisa. Raia wa nchi hizo anajinunulia tiketi yake na kujiendea sehemu yoyote Ufaransa, anajikodia nyumba apendapo na kuanza kujitafutia kazi. Yeye hahitaji idhini ya kuingia, kukaa au kazi. Je, ni kwa kiasi gani tunaweza kutetea uhalali wa uwepo wa tofauti hizi?

Pengine uwepo wa mipaka baina ya nchi na nchi unaweza kutetewa kama nyenzo madhubuti ya kuchuja uingiaji holela wa watu wasiostahiki kama vile magaidi na watoroshaji wa binadamu. Bali hali ni tofauti kabisa, maana wale wanaozuiwa kuingia katika nchi fulani kwa kanuni kali za uhamiaji na viza ni watu wa kawaida, wasio na jinai yoyote, wapenda amani ambao madhumuni yao ni kujitafutia maisha bora tu. Watu hawa hawazuiwi kwa vile wanaonekana ni watu wa hatari, la hasha, bali ni kwa sababu ya uzao wao ulipotokea. Hivyo basi, pale ambapo patakosekana sababu za msingi za ‘ubaguzi’ huo, tunaweza kusema kwamba maadili yanakiukwa mno. Kadhia hii ya ubaguzi na unyanyasaji unaathiri haki ya usawa baina ya wanadamu na pia inakiuka haki za mamilioni ya watu duniani kwa kuwanyima fursa za kuboresha maisha yao. Kwa mfano, mfanyakazi wa kawaida huko Ufaransa analipwa Euro 1500 kama kima cha chini kwa mwezi. Hii ni sawa na shillingi milioni nne za Kitanzania, yaani mara kumi hadi hamsini ya kipato cha Mtanzania. Mipaka huru huleta manufaa makubwa. Wanauchumi wanaamini kwamba nchi zenye mipaka huru zinaweza kujiongezea pato la taifa (GDP) maradufu. Kwenye makala ya jarida maarufu la The Economist ilikadiriwa kuwa endapo mipaka ingekuwa huria basi dunia ingejiongezea utajiri wa dola trilioni 78. Makala inasema “watu huongeza ufanisi katika uzalishaji pale wanapohajiri kutoka nchi masikini na kuhamia kwenye nchi tajiri. Haraka huingia kwenye soko la ajira lenye mtaji, makampuni yenye ufanisi na yenye sheria madhubuti zinazotabirika hufaidika. Wale waliokuwa wakitumia jembe la mkono sasa wanaanza kuendesha matrekta. Wale waliokuwa wakifyatua matofali kwa mikono wanaanza kuendesha krini na kuongoza magari ya uchimbaji. Na wale vinyozi wananza kupata wateja matajiri watoao bahshishi nono. Vizuizi vilivyopo kwenye soko huria la kazi ni moja katika vizuizi vibaya kabisa vinavyozuia ukuaji wa uchumi wa dunia kwa jumla. Endapo vizuizi hivi vitaondoshwa basi hii itakuwa programu ya pekee na ya aina yake ya kupambana na umasikini ambayo imeweza kuwahi kubuniwa.

Mistari ya mipaka inayogawanya uso wa dunia, nyaya za umeme, kuta ndefu, kamera, droni na walinzi wenye silaha kila sehemu ni uthibitisho tosha kuwa mwanadamu amefikia kilele cha udhalili kinacholeta tahayuri kuu ya kimaadili juu ya utu wa mwanadamu. Pale ambapo tunatakiwa tuwe huru kuitembea dunia ambayo sote sisi ni warithi wake kwa mizani sawa, tunajifunga wenyewe kwa kujiwekea sheria ngumu za uhamiaji na viza zinazodhalilisha, kuhatarisha, kukandamiza na za kibaguzi ambazo hazitegemewi kamwe kuweza kuleta maslahi yoyote zaidi ya maangamizi. Madhali kuna wanasiasa kama Donald Trump na Viktor Orban wanaoshinda chaguzi zao kwa kupenyeza hisia kali dhidi ya wahamiaji nachelea kusema kwamba ndoto ya kuwa na dunia isiyo na mipaka itabaki kama njozi tu kwa sasa. Ila matumaini yangu bado yanabaki kwa raia vijana wanaoamini kuwa mabadiliko yanahitajika ili kuleta dunia yenye usawa na haki kwa wote.

Imetafsiriwa na Masoud Nassor


A version of this article was published under the following title:
“Mipaka ya kijiografia isiwe chanzo cha ubaguzi na udhalili,” Mwananchi (Tanzania, 30 November 2018)