Kupiga watoto sio sawa

Isipokuwa kama unajilinda mwenyewe au unamlinda mtu mwingine, kumpiga mtu ni shambulio, na shambulio ni kinyume cha sheria. Hakuna mjadala juu yake, na hakuna sababu nzuri sana kwa nini iwe hivyo. Watu wana haki ya kuheshimiwa. Kumpiga mtu sio tu husababisha maumivu ya mwili – ni udhalilishaji. Ndiyo maana ni nchi chache tu ambazo bado zinatumia mateso ya kimwili kama adhabu. Tunaposoma makala za habari kuhusu nchi zinazowapiga watu viboko kwa uharibifu wa kitu fulani au kuiba, wengi wetu hukwazika na kushangaa: “Ni unyama ulioje!” Tumechoka na kuchoshwa na vurugu. Ubinadamu umepitia mambo mabaya mengi sana, na imekuwa nadra sana kwa binadamu kufanya mambo mema. Vurugu inapaswa kuwa suluhu ya mwisho, na itumike tu inapobidi.

Cha kustaajabisha, kuna kundi la watu ambao wameacha kushughulika na mambo yanayoleta amani na kuzuia vurugu. Watoto ulimwenguni pote “hupigwa,” “huchapwa,” na “hucharazwa” na wazazi na walimu ambao wanakabiliana na upinzani mdogo kutokana na mazoea hayo kukubalika na jamii. Ulimwenguni kote, takribani watoto bilion moja – yaani, 6 kati ya 10 – wenye umri kati ya miaka 2 na 14 wanapata adhabu ya kimwili mara kwa mara, kutoka kwa walezi wao na kufanya adhabu ya kimwili kuwa aina ya kawaida ya ukatili dhidi ya watoto. Je, si unafiki kushutumu mtu mzima kwa kumpiga mtu mzima mwingine, na serikali kwa kuwatesa kimwili wahalifu kama adhabu, ilhali zinaridhia “kupigwa,” “kuchapa,” na “kucharazwa viboko” kwa watoto nyumbani na shuleni? Ingawa neno “kuchapa” linatumika badala ya neno “kupiga” ili kupunguza makali, kuchapa watoto ni saw ana kuwapiga tu, na ikumbukwe watoto ni watu (na sio mali ya watu wazima; awe mzazi, mlezi au mwalimu), hivyo kumpiga mtoto ni kumpiga mtu. Ikiwa tunafikiri kwamba ni kinyume cha sheria kuwapiga hata wale watu wazima ambao wamefanya uhalifu, kwa nini watu wengi wanaona ni sawa kutoa adhabu za mateso ya kimwili dhidi ya watoto? Je, ni kwa kuwa ni kundi lisilo nguvu zaidi katika jamii? Je, watoto hawastahili ulinzi zaidi kuliko watu wazima?

Adhabu ya kimwili kwa watoto hufanyika kwa njia nyingi. Kuna matukio ya kutisha zaidi, kama vile baba mlevi kumpiga mtoto wake kwa sababu analia mara kwa mara bila kutambua kuwa mtoto huyo ni mdogo sana kuelewa kwa nini anaadhibiwa. Lakini hatukatai pia kuna matukio ambayo wazazi au walimu huwapiga watoto kwa nia njema. Mara nyingi mada hii inapotokea, bila shaka atatokea mtu na kusema: “Nilikuwa nikipigwa sana nikiwa mtoto na ikanisadia kuwa mtu mzuri nilipokuwa!” – Ni kweli, sio watoto wote wanaopata adhabu ya kimwili watakuwa watu wa hovyo ukubwani. Lakini hii haifanyi hoja ya watoto kupigwa kuwa nzuri. Tuchukulie mfano, baadhi ya wanawake wajawazito hunywa pombe na kuzaa watoto wenye afya nzuri kabisa; Je, kwa mantiki hii ni wazo nzuri kwa wanawake wajawazito kunywa pombe angalau mara moja moja? Si kweli! Hadithi kama hizi mara chache hutoa ushahidi wa kuaminika. Maamuzi sahihi yanatokana na sayansi, na tuna utafiti wa miongo kadhaa unaoonyesha kuwa watoto wanaochapwa wana uwezekano mkubwa wa kupata matatizo ya afya ya akili na matatizo ya kujifunza, na wana uwezekano mkubwa wa kushiriki katika tabia zisizofaa katika kijamii wakiwa watu wazima, ikiwa ni pamoja na tabia ya uhalifu. Kama kwa sasa wewe ni mtu mzuri, haimaanishi kuwa wazazi au walimu wako walikupiga sana wakati ukiwa mtoto. La hasha!

Uhusiano mzuri kati ya mzazi na mtoto unategemea upendo na uaminifu. Wazazi wanapowapiga watoto wao, huzua hisia kama vile woga na aibu, ambazo si sumu tu kwa uhusiano na watoto wao, bali pia hutia sumu katika mahusiano ya baadaye ya watoto wao na wengine. Watoto wanaojifunza nyumbani kwamba ukatili ni njia inayokubalika ya kusuluhisha mizozo wana uwezekano mkubwa wa kuwa wahasiriwa wa uhalifu wao wenyewe wanapokuwa wakubwa. Uhalifu huu zaidi ni sana unajumuisha unyanyasaji wa wenza wao, jambo ambalo limekuwa tatizo kubwa na la kutisha la afya ya umma. Maneno ya hekima yanapotamkiwa kwa watoto, yanafaa sana kaatika kukabiliana na tabia isiyotakikana kwa watoto, badala adhabu ya kimwili yenye madhara ya muda mrefu.

Ukifuatilia suala hili katika maeneo mengi ambapo kupiga watoto ni jambo lililoenea sana – na linalokubalika na watu wengi – kama hali halisi ya kijamii, unaweza kushawishika kuwa mtazamo huu hauzuiliki: “Na wazazi wataendelea kuwapiga watoto wao kila mara, na watafanya hivyo daima kwa sababu ni sehemu ya utamaduni na maadili yetu.” Hata hivyo tamaduni na maadili, siyo amri za Mungu tuseme hazibadiliki. Zinabadilika kila wakati. Mabadiliko hayo kwa kawaida huwa ya polepole, ndiyo maana huwa hatuyatambui, lakini nenda tu uzungumze na watu ambao wamekuzidi umri kwa miongo michache, na watakuambia ni kiasi jamii imebadilika tangu wakiwa wadogo. Mnamo 1979, Uswidi ilikuwa nchi ya kwanza kupiga marufuku adhabu zote za viboko kwa watoto, mashuleni pamoja na nyumbani. Wakati huo, 90% ya wazazi nchini Uswidi walipiga watoto wao. Mnamo mwaka wa 2000, namba hiyo ilipungua hadi kufikia 10% na chini zaidi hii leo. Wakati mwingine, inachukua kizazi kimoja tu kubadili utamaduni! Ingawa mabadiliko hayaji yenyewe. Tunahitaji kuweka mambo katika njia ifaayo sasa, kuelekea wakati ujao ambapo watoto watakua bila vurugu.