Falsafa ya Haki za Wanyama


Msimamo wa Haki za Wanyama

Wanyama wengine ambao binadamu huwatumia kwa chakula, katika sayansi, huwawinda, huwakamata, na kuwanyanyasa kwa namna mbalimbali, wana maisha yao binafsi ambayo yana thamani kwao wenyewe na sio tu kwa sababu ya matumizi yao kwetu. Sio tu kwamba wapowapo duniani, bali wanaufahamu. Wanachokipitia kina maana kwao. Kila mnyama ana maisha ambayo yanaweza kuwa mazuri au mabaya kulingana na namna anavyotendewa.

Maisha hayo yanajumuisha aina mbalimbali za mahitaji ya kibiolojia, ya kibinafsi, na ya kijamii. Mahitaji haya yakitimia huleta furaha, lakini yakipuuzwa au yakikosekana husababisha maumivu. Kwa misingi hii, wanyama wasio binadamu kama wale walioko kwenye maabara na kwenye mashamba, wapo sawa na binadamu. Kwa hiyo, maadili yanayoongoza namna tunavyowatendea wanyama, na jinsi tunavyotendeana sisi kwa sisi, yanapaswa kuzingatia kanuni zile zile za msingi za kimaadili.

Maadili ya binadamu ukiyatazama katika kiini chake kabisa, yanajengwa na thamani ya ndani ya mtu binafsi: Thamani ya kimaadili ya binadamu yeyote haipaswi kupimwa kwa kuangalia mtu huyo ni muhimu kwa kiasi gani katika kuendeleza maslahi ya binadamu wengine. Kuwatendea binadamu kwa njia zisizoheshimu thamani yao ya asili ni kukiuka haki ya msingi kabisa ya binadamu: haki ya kila mtu kutendewa kwa heshima.

Falsafa ya haki za wanyama inahitaji tu kwamba mantiki hiyo iheshimiwe. Kwa kuwahoja yoyote inayoweza kuelezea kwa kimantiki, thamani ya asili ya binadamu pia ina maana kwamba wanyama wengine nao wana thamani hiyo hiyo, na wanayo kwa kiwango sawa. Na hoja yoyote inayoweza kuelezea haki ya binadamu ya kutendewa kwa heshima pia inaashiria kwamba wanyama hawa wengine wana haki hiyo hiyo, na wanayo kwa usawa huo huo pia.

Ni kweli basi, kwamba wanawake hawakuumbwa ili kuwatumikia wanaume, watu weusi kuwatumikia watu weupe, maskini kuwatumikia matajiri, wala wanyonge kuwatumikia wenye nguvu. Falsafa ya haki za wanyama sio tu kwamba inaukubali ukweli huu, bali pia inauunga mkono na kufafanua ni kwanini ukweli huu ni sahihi. Lakini falsafa hii haishii hapo, inaenda mbali zaidi. Kwa kutambua kuwa wanyama wengine pia wana thamani ya asili na haki zao binafsi, falsafa hii inatoa sababu za kisayansi na zisizo na upendeleo wa kimaadili za kukataa wazo kwamba wanyama wapo ili kutunufaisha sisi binadamu.

Mara tu ukweli huu unapotambuliwa, inakuwa ni rahisi kuelewa kwa nini falsafa ya haki za wanyama haiyumbishwi katika kukabiliana na kila aina ya ukatili wanaofanyiwa wanyama wengine. Haki hiyo haimaanishi kuwa na mabanda makubwa au masafi zaidi kwa wanyama wanaotumiwa kwenye tafiti za kisayansi, bali inataka mabanda hayo yabaki tupu kabisa; haitetei “ufugaji wa kienyeji” wa wanyama, bali inadai kukomeshwa kabisa kwa biashara zote za kuuza nyama za wanyama waliokufa; wala haikubaliani na kuwepo kwa uwindaji au ukamataji wa wanyama ambao ni “wa kibinadamu” zaidi, bali inataka kutokomeza kabisa vitendo hivi vya kikatili.

Kwa sababu pale ambapo ukatili unapokuwa ni wa kiwango cha juu kabisa, basi unapaswa kupingwa kwa kiwango cha juu. Haki haikuwahi kudai “marekebisho” kwenye utumwa, wala haikuwahi kudai “marekebisho” katika ajira za watoto, wala haki haikuwahi kudai “marekebisho” kwa namna wanawake walivyonyanyaswa. Katika kila mojawapo ya hali hizi, jibu pekee ambalo ni sahihi kimaadili ni utokomezaji kabisa wa dhuluma hizi. Kujaribu kufanya marekebisho ya dhuluma za aina hii zenye ukatili wa kiwango cha juu ni kuendelea kuongeza ukatili.

Falsafa ya haki za wanyama inadai jibu hilo hilo – utokomezaji – kama jibu la unyanyasaji wa haki za wanyama wengine. Sio vipengele tu vya unyonyaji huo usio na haki vinavyopaswa kubadilishwa, ni unyonyaji wote wa haki yenyewe ambao lazima ukomeshwe, iwe ni kwenye mashamba, katika maabara, au porini. Falsafa ya haki za wanyama haiombi zaidi ya hapo, lakini pia haitaridhika na chochote kilicho chini ya utokomezaji.


Sababu 10 za Kutetea Haki za Wanyama na Maelezo Yake

1. Falsafa ya haki za wanyama ina busara.

Maelezo: Sio jambo la busara kubagua bila sababu ya msingi. Kuwabagua wanyama wasio binadamu ni ubaguzi usio na busara. Tunajua kuwa ni kosa kuwatendea binadamu walio dhaifu – hasa wale wasio na uwezo wa kawaida wa kufikiri – kama “vitu ama zana”, au “bidhaa”. Kwa hiyo, kama ni kosa kuwatendea wanadamu, basi haiwezi kuwa sahihi kuwatendea wanyama wengine kama “vitu ama zana” au “bidhaa” pia, ilihali wana hisia na maisha na saikolojia inayofanana au hata kuzidi ya binadamu hao. Kufikiri vinginevyo ni kukosa busara.

“Kumwelezea mnyama kama kiumbe tu aliyeundwa na mifumo mingi ya kikemikali ambae yuko hai ni sahihi kabisa, isipokuwa maelezo hayo yanashindwa kueleza hali halisi ya kuwa mnyama.” – E. F. Schumacher

2. Falsafa ya haki za wanyama ina msingi wa kisayansi.

Maelezo: Falsafa ya haki za wanyama kwa ujumla inaheshimu na kuzingatia ushahidi wa sayansi yetu bora ya kisasa, hasa biolojia ya mabadiliko ya asili. Biolojia hiyo inatufundisha kwamba, kama Charles Darwin alivyosema, binadamu na wanyama wengine wengi kiasili wanafanana, tofauti iliyopo si ya kimsingi bali ni ya kiwango na si ya aina. Bila kuingia kwa undani katika mipaka halisi ya tofauti hizo, ni dhahiri kwamba wanyama wanaotumiwa katika maabara, wanaofugwa kwa ajili ya chakula, au wanaowindwa kwa burudani au kunaswa kwa madhumuni ya kibiashara, ni ndugu zetu wa karibu kisaikolojia. Hoja hii si ya kubuniwa au ya kihisia; ni ukweli uliothibitishwa kwa ushahidi thabiti wa kisayansi.

“Hakuna tofauti ya kimsingi kati ya wanadamu na mamalia wa juu katika uwezo wao wa kiakili.” – Charles Darwin

3. Falsafa ya haki za wanyama haina ubaguzi.

Maelezo: Wabaguzi wa rangi ni watu wanaoamini kwamba wanajamii wenye rangi kama yao ni bora kuliko wanajamii wa rangi nyingine, kwa sababu tu wao wanatoka katika jamii ya watu hao, wanayoiona kuwa “bora”. Vivyo hivyo, wabaguzi wa kijinsia huamini kwamba watu wa jinsia yao ni bora kuliko watu wa jinsia nyingine, kwa sababu tu wao wanatoka katika jinsia hiyo wanayoiona kuwa “bora”. Ubaguzi wa rangi na ubaguzi wa kijinsia ni mifano dhahiri ya chuki isiyo na msingi wa kiakili au kimantiki. Hakuna rangi wala jinsia iliyo “bora” au “duni.” Tofauti za rangi na za kijinsia ni tofauti za [kijamii na] kibiolojia, si tofauti za kimaadili.

Hivyo hivyo ndivyo ilivyo kwa ubaguzi wa kispishi (speciesism) – mtazamo kwamba viumbe wa spishi ya mwanadamu (Homo sapiens) ni bora kuliko viumbe wa spishi nyingine zote, kwa sababu tu binadamu yeye yupo katika spishi anayoiona kuwa “bora”. Kwa kuwa hakuna spishi iliyo “bora” kimaadili, kimsingi kuamini vinginevyo ni kudumisha ubaguzi usio na utofauti na ubaguzi wa rangi au wa kijinsia.

“Ikiwa unaweza kuhalalisha kuua ili kula nyama, basi unaweza pia kuhalalisha hali za maisha duni ya watu wanaoishi kwenye mazingira magumu (ghetto). Mimi siwezi kuhalalisha hata kimoja kati ya hivyo.” – Dick Gregory

4. Falsafa ya haki za wanyama ni ya haki.

Maelezo: Katika maadili, haki ndio kanuni ya juu kabisa. Kwa mujibu wa kanuni hii, haipaswi kutenda wala kuruhusu dhuluma kufanyika hata kama italeta matokeo mazuri yenye faida, wala si sawa kukiuka haki za wachache ili wengi wanufaike. Utumwa ulihalalishwa kwa hoja kama hizo. Kutumikisha watoto kulihalalishwa vivyo hivyo. Mifano mingi ya dhuluma za kijamii imejengwa juu ya mantiki hiyo potofu. Hata hivyo, falsafa ya haki za wanyama haikubali msimamo huo. Kanuni yake ya msingi ni haki: hakuna mtu aliye na haki ya kufaidika kutokana na ukiukwaji wa haki za mwingine, iwe huyo “mwingine” ni binadamu au mnyama mwingine yeyote.

“Sababu za kuingilia kati kisheria kwa ajili ya kuwalinda watoto zinatumika kwa nguvu ile ile, na kwa kiasi kile kile kwa waliokuwa watumwa wasio na bahati – yaani wanyama (wengine).” – John Stuart Mill

5. Falsafa ya haki za wanyama ni ya huruma

Maelezo: Maisha ya binadamu yaliyokamilika yanahitaji uwezo wa kuhisi uchungu na mateso ya wengine na kuwajali – yaani, kuwa na huruma kwa waathirika wa dhuluma, iwe ni binadamu au wanyama wengine. Katika muktadha huu, falsafa ya haki za wanyama inahimiza kuwa na fadhila ya huruma, na kukubalika kwake kutasaidia kukuza zaidi hilo kwa ukamilifu. Falsafa hii ni, kwa maneno ya Lincoln, ndiyo “njia ya mwanadamu aliyekamilika.”

“Huruma inapowekwa katika vitendo inaweza kuwa ndilo tumaini kuu linaloweza kuilinda sayari yetu iliyojaa watu, na kukabiliwa na changamoto za uchafuzi wa mazingira…” – Victoria Moran

6. Falsafa ya haki za wanyama haina ubinafsi.

Maelezo: Falsafa ya haki za wanyama inahitaji kujitoa kuwatumikia wale ambao ni dhaifu na walio hatarini – wale ambao, iwe ni binadamu au wanyama wengine, hawana uwezo wa kuzungumza au kujitetea, na ambao wanahitaji ulinzi dhidi ya tamaa na uovu wa binadamu. Falsafa hii inahitaji kujitolea kwa namna hii, si kwa sababu ni kwa maslahi yetu binafsi kufanya hivyo, bali kwa sababu ni sahihi kufanya hivyo. Kwa hiyo, falsafa hii inahimiza kuwahudumia wengine bila kuwa na ubinafsi, na kupokelewa kwake kutasaidia zaidi ukuaji wa huduma hiyo isiyo na ubinafsi.

“Tunahitaji falsafa ya maadili ambayo dhana ya upendo, ambayo siku hizi huwa inatajwa mara chache sana na wanafalsafa, iweze tena kuwa mada kuu.” – Iris Murdoch

7. Falsafa ya haki za wanyama inajikidhi yenyewe.

Maelezo: Tamaduni zote kuu katika maadili, za kidini na zisizo za kidini, zinasisitiza umuhimu wa vitu vinne: maarifa, haki, huruma, na uhuru wa kufanya maamuzi binafsi. Falsafa ya haki za wanyama inafundisha hivyo hivyo. Falsafa hii inafundisha kwamba maamuzi yetu yanapaswa kuchukuliwa kwa kuzingatia maarifa, yanapaswa kuonyesha huruma na haki, na yanapaswa kufanywa kwa hiari. Si rahisi kuishi kwa misingi hii, wala si rahisi kudhibiti matamanio ya kibinadamu ya tamaa na kutojali. Lakini maisha kamili ya binadamu hayawezekani bila fadhila hizo. Falsafa ya haki za wanyama inahimiza ustawi wetu binafsi, na kupokelewa kwake kutakuza hilo.

“Ubinadamu sio tabia ya nje iliyokufa, bali ni msukumo hai kutoka ndani; sio majitoleo binafsi, bali ni kujitimiza.” – Henry Salt

8. Falsafa ya haki za wanyama ni ya maendeleo ya kijamii.

Maelezo: Kizuizi kikuu cha ukuaji wa jamii ya binadamu ni unyonyaji wa wanyama wengine unaofanywa na mikono ya binadamu. Hili linaonekana wazi katika lishe zisizokuwa na afya, matumizi ya wanyama wazima kama “mfano kamili wa majaribio” katika sayansi, na katika aina nyingine nyingi za unyonyaji wa wanyama. Pia inaonekana katika elimu na matangazo, kwa mfano, ambayo husaidia kupunguza hisia za binadamu na kushusha uwezo wa kufikiri, kujali, kuwa na huruma, na kutenda haki. Kwa njia zote hizi (na nyingine nyingi), mataifa hubaki nyuma kimaendeleo kwa kuwa yanashindwa kudumisha maslahi halisi ya raia wake.

“Ukubwa wa taifa na maendeleo yake ya kimaadili vinaweza kupimwa kwa jinsi wanyama wake wanavyotendewa.” – Mahatma Gandhi

9. Kimazingira, falsafa ya haki za wanyama ni yenye busara.

Maelezo: Sababu kuu ya uharibifu wa mazingira, ikiwa ni pamoja na ongezeko la joto duniani, uchafuzi wa vyanzo vya maji, na kupotea kwa ardhi yenye rutuba na mmomonyoko wa udongo, kwa mfano inaweza kuelezewa kutokana na unyonyaji wa wanyama. Mtindo huo huo unaonekana katika matatizo mengine mengi ya mazingira, kuanzia mvua ya asidi na utupaji wa taka zenye sumu baharini, hadi uchafuzi wa hewa na uharibifu wa makazi ya asili. Katika hali zote hizi, kuchukua hatua za kuwalinda wanyama walioathirika (ambao, siku zote, wao ndio wa kwanza kuteseka na kufa kutokana na matatizo haya ya mazingira), ni sawa na kuilinda dunia.

“Hadi pale tutakapojenga undugu wa kweli kati ya binadamu na viumbe wa jamii zingine wanaoishi pamoja na sisi chini ya jua katika sayari hii iliyojaa maumivu, hatutakuwa na tumaini kwa mazingira na hatutakuwa na matumaini kwetu wenyewe.” – Jon Wynne-Tyson

10. Falsafa ya haki za wanyama ni ya kupenda amani.

Maelezo: Msingi wa falsafa ya haki za wanyama ni kuwatendea binadamu na wanyama wengine kwa heshima. Kufanya hivyo kunahitaji tusiwadhuru wengine ili sisi wenyewe au wengine tupate faida. Kwa sababu hiyo, falsafa hii inapinga kabisa ukatili wa kijeshi. Ni falsafa ya amani. Lakini ni falsafa inayopanua mahitaji ya amani zaidi ya mipaka ya spishi yetu. Kwa kuwa kuna vita vinavyofanyika, kila siku, dhidi ya mamilioni ya wanyama wasio binadamu. Kusimamia kweli kwa ajili ya amani kunamaanisha kusimama imara dhidi ya ubaguzi wa kispishi. Ni kuwa na matumaini yasiyo ya kweli kuamini kwamba kunaweza kuwa na “amani duniani” ikiwa tutashindwa kuleta amani katika uhusiano wetu na wanyama wengine.

“Ikiwa kwa miujiza fulani katika jitihada zetu zote dunia itaepushwa na maangamizi ya nyuklia, ni haki kwa kila kiumbe hai pekee ndio itakayookoa binadamu.” – Alice Walker


Sababu 10 Dhidi ya Haki za Wanyama na Majibu Yake

1. Si sahihi kuwaweka wanyama na binadamu katika hadhi sawa, ilihali kwa hakika binadamu na wanyama hutofautiana kwa kiasi kikubwa.

Jibu: Hatusemi kwamba binadamu yuko sawa na wanyama kwa kila namna. Kwa mfano, hatusemi kwamba mbwa na paka wanaweza kufanya hesabu, au kwamba nguruwe na ng’ombe hufurahia wanaposikiliza mashairi. Tunachosema ni kwamba, kama binadamu, wanyama wengine nao pia ni viumbe wenye maisha ya ndani ya kiakili na kisaikolojia, ni viumbe wenye ustawi wao wa kimaisha unaotokana na uzoefu wao wenyewe. Kwa maana hii, basi, licha ya tofauti zetu nyingi, sisi na wao tuna hadhi sawa.

“Hoja zote za kuthibitisha ubora wa binadamu haziwezi kubatilisha ukweli huu mgumu: katika kuteseka/kuhisi maumivu, wanyama ni sawa na sisi.” – Peter Singer

2. Ni jambo la ajabu kusema kwamba, kila binadamu na kila mnyama wana haki sawa. Kuku hawawezi kuwa na haki ya kupiga kura, wala nguruwe hawawezi kuwa na haki ya kupata elimu ya juu.

Jibu: Hatusemi kwamba binadamu na wanyama wengine siku zote wana haki sawa. Hata binadamu wote hawana haki sawa. Kwa mfano, watu wenye matatizo ya ulemavu mkubwa wa kiakili hawana haki ya elimu ya juu. Tunachosema ni kwamba hawa pamoja na binadamu wengine wanashiriki haki ya msingi ya kimaadili na wanyama wengine – yaani, haki ya kutendewa kwa utu/heshima.

“Hatima ya kila ukweli ni kubezwa wakati unapotangazwa kwa mara ya kwanza.” – Albert Schweitzer

3. Ikiwa wanyama wana haki, hata mboga zina haki pia, jambo ambalo ni la kipuuzi.

Jibu: Wanyama wengi ni kama sisi: wana ustawi wao wa kisaikolojia. Kama sisi, kwa hiyo, wanyama hawa wana haki ya kutendewa kwa utu/heshima. Kwa upande mwingine, hatuna sababu, hasa ya kisayansi ya kuamini kwamba, kwa mfano, karoti na nyanya vina uwepo wa maisha yeyote ya ndani ya kiakili na kisaikolojia duniani. Kama mboga zingine zote, karoti na nyanya hazina chochote kinachofanana na ubongo au mfumo mkuu wa neva. Kwa sababu ya upungufu huu, hakuna sababu ya kufikiri kwamba mboga ni viumbe wenye maisha ya kiakili na kisaikolojia, wenye uwezo wa kuhisi furaha na maumivu. Kwa misingi hii, tunaweza kuthibitisha kwa hoja za kimantiki kuwepo kwa haki kwa wanyama na kuzikataa kwa mboga.

“Hoja ya haki za wanyama inategemea tu na uwezo wa kuhisi maumivu au furaha.” – Andrew Linzey

4. Je, unaweka mpaka wapi? Ikiwa nyani na panya wana haki, basi hata konokono na amiba wana haki pia, jambo ambalo ni la kipuuzi.

Jibu: Mara nyingi si rahisi kujua hasa ni wapi pa “kuweka mpaka huu.” Kwa mfano, hatuwezi kusema kwa usahihi kabisa mtu anapaswa kuwa na umri gani ili aitwe mzee, au ni urefu gani mtu akiwa nao ataitwa mrefu. Hata hivyo, tunaweza kusema kwa uhakika kwamba mtu mwenye umri wa miaka themanini na minane ni mzee, na kwamba mtu mwenye urefu wa futi saba na inchi moja (7’1”) ni mrefu. Vivyo hivyo, hatuwezi kusema kwa usahihi kabisa ni wapi pa kuweka mpaka linapokuja suala la wanyama wenye maisha ya ndani ya kiakili na kisaikolojia. Lakini tunaweza kusema kwa uhakika kamili kwamba, popote ambapo mpaka huo utakapowekwa kwa misingi ya kisayansi, nyani na panya watakuwa upande mmoja (upande wa viumbe wenye maisha ya ndani ya kiakili na kisaikolojia), ilihali konokono na amiba wako upande wa pili, ingawa hilo halimaanishi kwamba tunaweza kuwaangamiza bila kufikiri.

“Katika mahusiano ya binadamu na wanyama, na maua, na vitu vyote vya uumbaji, kuna maadili makubwa ambayo bado hayajaonekana kikamilifu.” – Victor Hugo

5. Lakini kwa hakika kuna baadhi ya wanyama wanaoweza kuhisi maumivu ila wanapungukiwa au kukosa maisha ya ndani ya kiakili au ya kisaikolojia. Kwa kuwa wanyama hawa hawana haki ya kutendewa kwa heshima/utu, falsafa ya haki za wanyama inathibitisha kwamba tunaweza kuwatendea kama tunavyotaka.

Jibu: Ni kweli kwamba baadhi ya wanyama, kama uduvi na chaza wa baharini, wanaweza kuwa na uwezo wa kuhisi maumivu lakini hawana uwezo mkubwa wa kisaikolojia kama wanyama wengine. Ikiwa hili ni kweli, basi watakosa baadhi ya haki ambazo wanyama wengine wanazo. Hata hivyo, hakuna uhalali wa kimaadili wa kumsababishia kiumbe mwingine yeyote maumivu ikiwa sio lazima. Na kwa kuwa si lazima binadamu wale kamba, chaza wa baharini, au wanyama kama hawa, wala kuwatumia kwa njia nyingine, basi hakuna uhalali wa kimaadili wa kuwasababishia maumivu ambayo yanaambatana na matumizi hayo.

“Swali si, ‘Je, wanaweza kufikiri?’ wala ‘Je, wanaweza kuongea?’ bali ‘Je, wanaweza kuhisi maumivu?’” – Jeremy Bentham

6. Wanyama hawaheshimu haki zetu. Kwa hivyo, binadamu hawana wajibu wa kuheshimu haki zao pia.

Jibu: Kuna hali nyingi ambapo mtu aliye na haki anashindwa kuheshimu haki za wengine. Hii ni kweli kwa watoto wachanga, watoto wadogo, na binadamu walio na ulemavu mkubwa wa akili au wagonjwa wa akili. Katika hali zao, hatusemi kwamba ni sawa kabisa kuwatendea bila utu/heshima kwa sababu hawaheshimu haki za wengine. Kinyume chake, tunatambua kwamba tuna wajibu wa kuwatendea kwa heshima, ingawa wao hawana wajibu wa kututendea kwa njia ile ile.

Kile ambacho ni kweli, kwa mfano huu wa watoto wachanga, watoto wadogo, na binadamu wengine waliotajwa, ni kweli pia kwa wanyama wengine. Hakika, wanyama hawa hawana wajibu wa kuheshimu haki zetu. Lakini hili haliondoi wala kupunguza wajibu wetu wa kuheshimu haki zao.

“Muda utakuja ambapo watu kama mimi watachukulia mauaji ya wanyama wengine kama wanavyochulia mauaji ya binadamu sasa kuwa ni kosa kimaadili.” – Leonardo Da Vinci

7. Mungu alimpa binadamu utawala juu ya wanyama wengine. Hii ndio sababu tunaweza kuwafanyia chochote tunachotaka, ikiwa ni pamoja na kuwala.

Jibu: Si dini zote zinamwonyesha binadamu kama wenye “utawala” juu ya wanyama wengine, na hata miongoni mwa zile zinazosema hivyo, dhana ya “utawala” inapaswa kueleweka kama mchungaji mwema, na si mtawala mwenye ubinafsi. Binadamu wanapaswa kuwa na upendo kwa viumbe vyote vilivyoumbwa kama vile Mungu alivyovipenda alipoviumba. Kama tungewapenda wanyama leo kwa namna binadamu alivyowapenda katika Bustani ya Edeni, tusingewala. Wale wanaoheshimu haki za wanyama wako katika safari ya kurudi Edeni – safari ya kurudi kwenye upendo wa kweli kwa uumbaji wa Mungu.

“Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu.” – Mwanzo 1:29

8. Ni binadamu pekee walio na roho zisizokufa. Hii inatupa haki ya kuwatendea wanyama wengine kama tunavyotaka.

Jibu: Dini nyingi zinafundisha kwamba wanyama wote, sio binadamu pekee, wana roho zisizokufa. Lakini, hata kama ni binadamu pekee ndio watakaoishi milele, hii ingethibitisha tu kuwa binadamu tunaishi milele wakati wanyama wengine hawaishi milele, na ukweli huu (ikiwa ni ukweli) unaongeza, badala ya kupunguza, jukumu letu la kuhakikisha kuwa maisha haya pekee waliyonayo wanyama yanakuwa ni marefu na bora kadiri inavyowezekana.

“Hakuna dini bila upendo, na watu wanaweza kuzungumza kadri wanavyotaka kuhusu dini yao, lakini ikiwa haitawafundisha kuwa wema na wema kwa wanyama wengine pamoja na binadamu, yote hayo ni udanganyifu.” – Anna Sewell

9. Ikiwa tunaheshimu haki za wanyama, na hatutawala au kuwatumia kwa njia nyingine, basi tutafanya nini na wanyama wote hawa watakaokuwa wamejaa? Ndani ya muda mfupi sana watajaa mitaani na majumbani mwetu.

Jibu: Kila mwaka, takriban wanyama bilioni 4-5 hufugwa na kuuawa kwa chakula, Marekani pekee [idadi hii ilipanda hadi kuwa zaidi ya bilioni 9 ya wanyama wanaoishi juu ya ardhi mwaka 2023; duniani kote, zaidi ya bilioni 85 ya wanyama wanaoishi juu ya ardhi huliwa kila mwaka, ambayo ni sawa na zaidi ya wanyama 2,500 kwa sekunde]. Sababu ya idadi hii kubwa sana ni rahisi: kuna wateja wanaokula kiasi kikubwa cha nyama. Ugavi wa wanyama unakidhi mahitaji ya wanunuzi.

Hata hivyo, falsafa ya haki za wanyama itakaposhinda, na watu wakawa walaji wa vyakula vinavyotokana na mimea, hatutapaswa kuogopa kuwa kutakuwa na mamilioni ya ng’ombe na nguruwe wakizurura katikati ya miji yetu au kwenye sebule zetu. Mara tu motisha ya kifedha ya kufuga mamilioni ya wanyama hawa itakapopotea, basi hawatafugwa kwa idadi hiyo. Mantiki hiyo hiyo inatumika pia sehemu zingine pia – kwa mfano, wanyama wanaofugwa kwa ajili ya utafiti. Falsafa ya haki za wanyama itakapokubalika na matumizi ya wanyama hawa yakasitishwa, basi motisha ya kifedha ya kuwafuga mamilioni yao pia itapotea.

“Dhambi mbaya zaidi dhidi ya viumbe wenzetu sio kuwachukia, bali ni kutokuwa na huruma kwao. Hicho ndiyo kiini cha ukatili.” – George Bernard Shaw

10. Hata kama wanyama wengine wana haki za kimaadili na wanapaswa kulindwa, kuna mambo muhimu zaidi ambayo yanahitaji umakini wetu – kama janga la njaa duniani, unyanyasaji wa watoto, ubaguzi wa rangi, dawa za kulevya, ukatili dhidi ya wanawake, na shida ya watu kukosa makazi. Baada ya kutatua matatizo haya, basi tunaweza kuanza kufikiria juu ya haki za wanyama.

Jibu: Harakati za haki za wanyama ni sehemu ya si tofauti na harakati za haki za binadamu. Falsafa ile ile inayodai na kulinda haki za wanyama wasio binadamu pia inadai na kulinda haki za binadamu.

Zaidi ya hayo, kwa mtazamo wa vitendo, chaguo ambalo watu wanaofikiri kwa makini wanakabiliana nalo si kati ya kusaidia binadamu au kusaidia wanyama wengine. Mtu anaweza kufanya yote mawili. Kwa mfano, watu hawahitaji kula wanyama ili kuwasaidia watu wasio na makazi, kama ambavyo hawahitaji kutumia vipodozi vilivyojaribiwa kwa wanyama ili kuwasaidia watoto. Kwa hakika, watu wanaoheshimu haki za wanyama wasio binadamu na kutowatumia kama chakula, huwa na afya bora zaidi, na hivyo wanakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuwasaidia binadamu pia hata zaidi.

“Ninaunga mkono haki za wanyama pamoja na haki za binadamu. Hiyo ndiyo njia ya ubinadamu kamili.” – Abraham Lincoln


Tafsiri: Wilson John Simon & Subira Ndutu

Kitabu hiki hapo awali kilichapishwa na kusambazwa na Culture & Animals Foundation. Tafsiri ya sasa imetengenezwa tena kwa idhini ya Culture & Animals Foundation. Maelezo zaidi kuhusu kazi zao yanapatikana kwenye cultureandanimals.org.

Maelezo yaliyo ndani ya mabano ya mraba yametolewa na mhariri.

Shukrani za pekee pia kwa Goodluck Gabriel Mosha kwa uhakiki wake makini wa tafsiri na ushauri wake wa thamani. Watafsiri wanawajibika peke yao kwa dosari au makosa.


Video zilizorekodiwa za Tom Regan

Katika Taasisi ya Royal Institution ya Uingereza mnamo 1989:

Chuo Kikuu cha Heidelberg nchini Ujerumani mnamo 2006:


Usomaji Zaidi

Orodha ifuatayo ya vitabu na machapisho ya kusoma zaidi si kamili. Majina ya vitabu pamoja na machapisho yaliyo kwa herufi nzito yanafaa zaidi hasa kwa wasomaji wapya wanaoanza kujifunza masuala ya maadili ya haki za wanyama.

Kiswahili

  • Peter Singer, Ukombozi wa Wanyama (Mkuki na Nyota, 2023), ISBN: 978-9987084913

Kiingereza

  • Carol J. Adams, The Sexual Politics of Meat: A Feminist-Vegan Critical Theory (Bloomsbury Academic, 2024), ISBN: 979-8765123669
  • Paola Cavalieri, The Death of the Animal: A Dialogue (Columbia University Press, 2009), ISBN: 978-0231145527
  • J. M. Coetzee, The Lives of Animals (Princeton University Press, 2016), ISBN: 978-0691173900
  • David DeGrazia, Animal Rights: A Very Short Introduction (Oxford University Press, 2002), ISBN: 978-0192853608
  • Sue Donaldson & Will Kymlicka, Zoopolis: A Political Theory of Animal Rights (Oxford: Oxford University Press, 2011), ISBN: 978-0199599660
  • Rainer Ebert, „Being a World Unto One’s Self: A Phenomenal Consciousness Account of Full and Equal Moral Status,“ Zeitschrift für Ethik und Moralphilosophie 5 (2022), pp. 179–202
  • Rainer Ebert & Anteneh Roba (Wahariri), Africa and Her Animals: Philosophical and Practical Perspectives (University of South Africa Press, 2018), ISBN: 978-1868889006
  • Gary L. Francione, Introduction to Animal Rights: Your Child or the Dog? (Temple University Press, 2000), ISBN: 978-1566396929
  • Lori Gruen, Ethics and Animals: An Introduction (Cambridge University Press, 2021), ISBN: 978-1108986571
  • Oscar Horta, Making a Stand for Animals (Routledge, 2022), ISBN: 978-1032259758
  • Melanie Joy, Why We Love Dogs, Eat Pigs, and Wear Cows: An Introduction to Carnism (Red Wheel, 2020), ISBN: 978-1590035016
  • Andrew Linzey, Animal Theology (University of Illinois Press, 1995), ISBN: 978-0252064678
  • Andrew Linzey & Clair Linzey (Wahariri), Animal Theologians (Oxford University Press, 2023), ISBN: 978-0197655573
  • Nathan Nobis, Animals & Ethics 101: Thinking Critically About Animal Rights (Open Philosophy Press, 2016), ISBN: 978-0692471289, available for free at animalethics101.com
  • Martha C. Nussbaum, Justice for Animals: Our Collective Responsibility (Simon & Schuster, 2024), ISBN: 978-1982102517
  • Evelyn B. Pluhar, Beyond Prejudice: The Moral Significance of Human and Nonhuman Animals (Duke University Press, 1995), ISBN: 978-0822316480
  • Tom Regan, The Case for Animal Rights (University of California Press, 2004), ISBN: 978-0520243866
  • Tom Regan, Empty Cages: Facing the Challenge of Animal Rights (Rowman & Littlefield, 2004), ISBN: 978-0742549937
  • Mark Rowlands, Animals Like Us (Verso Books, 2002), ISBN: 978-1859843864
  • Mark Rowlands, Animal Rights (MIT Press Essential Knowledge, 2025), ISBN: 978-0262549400
  • Jeff Sebo, The Moral Circle: Who Matters, What Matters, and Why (W. W. Norton & Company, 2025), ISBN: 978-1324064800
  • Peter Singer, Animal Liberation Now: The Definitive Classic Renewed (Harper Perennial, 2023), ISBN: 978-0063226708
  • Cass R. Sunstein & Martha C. Nussbaum (Wahariri), Animal Rights: Current Debates and New Directions (Oxford University Press, 2004), ISBN: 978-0195305104
  • Steven M. Wise, Rattling The Cage: Toward Legal Rights For Animals (Perseus Publishing, 2000), ISBN: 978-0738204376
  • Steven M. Wise, Drawing the Line: Science and the Case for Animal Rights (Basic Books, 2003), ISBN: 978-0738208107

Maelezo ya Wasifu

Dk. Tom Regan alikuwa mtu mkarimu na mwenye moyo wa upendo, na rafiki wa wengi. Alikuwa mwanafalsafa kwa taaluma na wito, aliunganisha kwa ustadi mkubwa nidhamu ya taaluma yake na umakini wake mkubwa katika mambo pamoja na shauku inayosambaa ya imani ya kimaadili. Maisha na kazi yake vilikuwa dira ambayo ilileta mwelekeo kwenye maisha ya wengi, na bado vitaendelea kuhamasisha vizazi vijavyo. Kwa wakati alipokuwa kijana, maisha yake mwenyewe yalibadilika baada ya kukutana na uandishi wa Mahatma Gandhi, tukio ambao lilianzisha safari yake mpya kutoka kuwa mlaji wa nyama hadi kuwa mtu anayekula vyakula vya mimea, na hatimaye kuwa mmoja wa watu mashuhuri zaidi wanaotetea haki za wanyama wasio binadamu katika kizazi chake.

Tom Regan alizaliwa Pittsburgh, Pennsylvania, tarehe 28 Novemba 1938. Alifundisha falsafa katika Chuo Kikuu cha North Carolina State kwa miaka 34. Aliandika zaidi ya vitabu ishirini – ikiwa ni pamoja na The Case for Animal Rights (1983) – na mamia ya makala za kitaaluma, ambapo ndani yake alifafanua kwa kina na kwa ustadi mkubwa mawazo ambayo yaliyoainishwa katika maandishi haya mikononi mwetu. Wasifu wake binafsi katika sehemu mbili, The Bird in the Cage: A Glimpse of My Life, ulichapishwa katika toleo la pili la Between the Species mnamo mwaka 1986. Kupitia mihadhara mingi duniani kote, aliwasaidia wasikilizaji, kuona ng’ombe, nguruwe, kuku, kondoo, mbuzi na wanyama wengine wasio binadamu kama viumbe wa kipekee, wenye thamani sawa na mimi na wewe. Alifariki huko Raleigh, North Carolina, mnamo Februari 17, 2017.